NDUGU WAGENI WAALIKWA, MABIBI NA MABWANA



Ninavyofahamu ni kwamba madhumuni ya Mfuko wa Uadilifu, Uwajibikaji na Uwazi ni kukuza uwezo wa taasisi na siyo kulipia gharama za uendeshaji. Kwa maana hiyo sitarajii Mfuko huo uwe unafadhili ununuzi wa magari, ulipiaji wa mishahara, posho, ujenzi na gharama nyingine za kiutawala za taasisi zinazohusika. Vile vile sitazamii kuwa mfuko utajihusisha na uwekezaji katika shughuli za kibiashara. Kwa hivyo, ni muhimu kwa walengwa wa Mfuko huo, kuwa makini kila wanapotayarisha maombi yanayohitaji ufadhili.

Walengwa wote, hawana budi kutilia maanani kwamba fedha za Mfuko zinazotolewa ni ufadhili, na wala si mkopo. Napenda kusisitiza tena. Mfuko huu haukuwekwa kwa ajili ya kulipia gharama za uendeshaji wa siku hadi siku wa shughuli za asasi na taasisi zo zote zinazolengwa. Kwa hivyo, natoa wito kwa wale wote ambao ni walengwa kuibua miradi yenye kukidhi vigezo vilivyowekwa, na ambayo itasaidia kutimiza malengo ya Mfuko wa Uadilifu, Uwajibikaji na Uwazi. Aidha, napenda pia kuwaasa watakaofadhiliwa na Mfuko huu kuhakikisha kuwa fedha wanazopewa kutoka hazina ya Mfuko zinatumiwa katika shughuli zilizokusudiwa kutekelezwa. Ni muhimu ifahamike mapema kuwa fedha za Mfuko huu ni fedha za umma. Kwa hivyo, matumizi yo yote ambayo yatakwenda kinyume na madhumuni yaliyokusudiwa ni sawa na ufujaji wa fedha za umma. Kwa vyo vyote hatua kali zikiwemo za kisheria itabidi zichukuliwe dhidi ya wale wote watakaohusika na ufujaji huo.

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Postagem Anterior Próxima Postagem