
Naamini watu hawajafumba macho dhidi ya serikali. Wanaona kila kitu na ndio maana wanakosoa, na sababu kubwa ya kukosoa ni kuwa wanaona kuna kila dalili ya kufanya vizuri, lakini hatufanyi vizuri.
Lowassa anakiri kuwa hatua tuliyofikia ni nzuri na inaonyesha ndege yetu ya kutafuta maisha bora kwa kila mtanzania imeanza kupaa na kwa jasho la Watanzania na kwa uongozi bora wa Serikali ya CCM chini ya Rais Kikwete, Tanzania inasonga mbele na dunia inaona na kukiri hivyo.
Hapa ndipo panapozua maswali mengi. Hivi tunafanya ili dunia itambue na kukiri au tunafanya kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo? Mbona wakati wa kampeni hakuna aliyewaahidi wananchi kuwa atajitahidi kuhakikisha kuwa anafanya vizuri hadi dunia itambue hivyo? Mbona, tumekuwa wepesi wa kushikilia takwimu za watu wa nje na kudai kuwa tunafanya vizuri katika maendeleo ya taifa letu? Inaniwia vigumu kuamini kama kweli viongozi wetu wanapotembelea maeneo ya vijijini, hupata fursa ya kuona miguu ya wananchi ambayo ina ukame wa kuvaa viatu, huku wao wakiwa na zaidi ya jozi 1,000. Huenda hilo hawalioni, maana wanakuwa katika magari na inakuwa vigumu kuanza kuangalia kama wananchi wao wamevaa viatu, lakini vipi kuhusu nyumba wanazoishi wananchi hao ambazo nyingi ni mbavu za mbwa? Ni maendeleo gani katika barabara tunayoyasema hapa? Hivi karibuni nilikuwa wilayani Tarime, jimbo ambalo lina utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu, lakini barabara zake zinatia aibu, wananchi wanalipa nauli utafikiri wanasafiri kwenda nje ya Mkoa wa Mara. Hivi kwa mwananchi wa Tarime, anaposikia maneno kama haya ya waziri mkuu anayapokea vipi? Atakuwa na furaha ati kwa sababu ni kiongozi wa nchi amesema au ataishia nae kulalama kuwa nchi hii tunadanganywa? Viongozi wetu badala ya kutafiti kiwango cha maendeleo kutoka kwa wananchi, ambao ndio walengwa, wanasubiri taarifa za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Hivi hao kuna siku watatukosoa wakati uchumi wote wa nchi uko mikononi mwao? Tutashangaa, lakini ukweli ni kwamba wataendelea kutusifu ili tuendelee kutegemea sera zao? Mbona wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere ambapo uchumi wetu ulikuwa imara walikuwa hawaishi kuikosoa serikali? Hapa ni vyema tukawa wajanja, wenzetu hao wanapokuja nchini huishia kusafiri katika barabara za Dar es Salaam, Arusha au Zanzibar ambazo ni nzuri. Je, watashindwa kusema kuwa tuna maendeleo katika sekta ya barabara? Wakati fulani kiongozi mmoja wa Serikali ya China alikuwa katika ziara hapa nchini na akataka kumtembelea Mwalimu Nyerere nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam. Kwa kuwa njia ilikuwa mbaya, serikali, kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, ikahangaika usiku kucha kuikwangua ili iweze kupitika. Mwalimu aliliona hilo na hakusita kulizungumzia. Alichosema ni kwamba, badala ya kuwadanganya wageni kuwa tuna barabara nzuri, ni vyema tuache wajionee hali halisi ili kama wanaweza kutusaidia, basi watusaidie kuzitengeneza. Kwa ushauri huo, ni vyema wakati mwingine watu wa IMF wanapokuja nchini wapate fursa ya kutembelea maeneo ya vijijini na kujionea wenyewe njia zetu ili tuone kama watathubutu kutuambia tunapiga hatua ya maendeleo katika sekta ya barabara. Narejea kwenye msisitizo aliouonyesha Waziri Lowassa kuwa, ndege yetu ya kutafuta maisha bora kwa kila Mtanzania imeanza kupaa. Hilo wala si tatizo, lakini tunapaswa kuuliza, ndege hiyo inapaa na kina nani? Ni Watanzania wa kada zote au ni tabaka la wenyenazo? Sambamba na hilo je, ikiishapaa itadumu angani kwa muda gani au ndiyo ikiishakaa usawa unaotakiwa basi inarudi chini kwa kasi ya ajabu? Muda mfupi kabla ya kuandika makala hii, nilikuwa nasoma juu ya kuanguka kwa ndege ya Shirika la Ndege la China katika Uwanja wa Naha uliopo Okinawa nchini Japan. Kwa mujibu wa shirika linalomiliki ndege hiyo, ndege hiyo ilikuwa nzima na haikuwa na tatizo lolote. Kwanini nilete mfano huo? Kwa sababu kuruka kwa ndege si hoja, ila jambo la msingi ni kwamba ndege hiyo ni nzima kiasi gani? Maana hata ndege mbovu zinaruka. Je, inaruka kuelekea wapi? Mheshimiwa Lowassa, sisi hatuna shaka juu ya ndege kuruka, ila tunajiuliza, inaruka na akina nani? Baada ya kuruka inachukua mweleko gani, na itadumu kuwa angani kwa muda mrefu? Kama majibu ni ndiyo, hakuna cha kugomba hapo, lakini kama hapana, basi fanyia kazi mawazo ya wanaopinga kwamba ndege haipai.