MKUU WA MKOA DODOMA AONJESHWA JOTO LA UCHAGUZI


KELELE za watu waliofika kwenye mkutano wa hadhara jana kumkataa mbunge wao Dk James Msekela ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, zilimlazimu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwauliza mara mbili kama kiongozi huyo atashinda tena, lakini wakajibu: "Aaa wapi, hashindi".

Baada wananchi nchi kupiga kelele za kumkataa mbunge huyo, Pinda aliwauliza wananchi hao akisema: "Je, Mbunge Msekela (Dk Alex) atashinda?" Wanakijiji cha Hiari ya Moyo-Kigwa "A", wilayani Uyui, Tabora wakajibu kwa sauti : "Aaa wapi, hashindi."

Akauliza tena swali hilo, na majibu yakawa hayo Hayo na kumfanya Waziri Mkuu asiendelee na maswali. Waziri Mkuu aliuliza wananchi ridhaa yao baada kusimama kwa muda kukagua shamba la tumbaku la mkulima mjane, Tabu Kisimba na kupokea maelezo ya yake pamoja na kuzungumza na wakulima wengine.

Pinda alianza kwa kuuliza kama wananchi wako tayari kuwapa kura viongozi wao wa sasa katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba mwaka huu ambao ni mbunge na diwani. "Je, Mko jtayari kumpa kura Diwani Mrisho Msambaki? Wananchi ambao bila hofu walijibu kwamba watampa kura diwani huyo.

Baada ya maswali kuhusu diwani huyo ndipo ilifika zamu ya Dk Nsekela ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma akiwauliza wananchi hao kama wako tayari kumpa kipindi kingine cha uongozi. Lakini wananchi hao walijibu kwa sauti ya juu wakisema: "hapana" .

Alipouliza tena waananchi hao walijizi kwa sauti za juu: "Aaa wapi, hashindi." Dk Nsekelela alipofuatwa kutoa maelezo juu ya tukio hilo alijipa moyo akisema, "Kama ulisikia kwa makini, wana CCM walijibu kuwa nitashinda, isipokuwa wale wa CUF ndio wanasema sitashinda."

Alidai kuwa wananchi waliosema hashindi waliongozwa na mfuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), aliyemtaja kwa jina la Mzee Khamis Mangurya.

Dk Nsekela alifafanua kuwa hizo ni siasa za kawaida ambazo hazikumuumiza na kwamba, ingawa ilitokea mbele ya Waziri Mkuu na kumsikitisha lakini, akasema atashinda tena kiti cha ubunge akisistiza yaliyotokea ndio siasa ilivyo.

Katika hatua nyingine naye Mbunge wa Igalula, Tatu Ntimizi ambaye hata hivyo hakuwapo katika ziara hiyo kutokana na kuugua ishara, wanannchi walionyesha hasira zao juu yake wake mbele ya Waziri Mkuu Pinda walikidai kuwa hakuonekana jimboni.

Katika ziara hiyo juzi usiku Pinda alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya viongozi wa serikali wanaotumia rasilimali za taifa kushabikia siasa na kujipatia umaarufu.

Waziri Mkuu alitoa onyo hilo mkoani Tabora alipo kwa ziara ya kikazi alisema aishapokea taarifa za malalamiko dhidi ya baadhi ya watendaji wanaotumia rasilimali za serikali kushabikia siasa.

"Baadhi ya watendaji ambao ni wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri hutumia rasilimali za serikali kushabikia siasa, alisema Pinda na kuongeza; "Viongozi hao waache kabisa mchezo huo kwani wao kama viongozi wa serikali siasa siyo jukumu lao, watakaobainika watachukuliwa hatua zote za kinidhamu."


Alisema ana taarifa za baadhi ya viongozi hao kujipitisha katika majimbo kutaka kuwania ubunge na wengine kuwapigia debe wagombea jambo alilosema si sahihi.

Aliongeza kuwa kwa kipindi hiki watu wanaotaka kuwania nafasi za uongozi wapo huru kutangaza nia zao na siyo kuanza kampeni. Waziri mkuu Pinda alisema wapo watu wanaotangaza kuwania nafasi hizo na kuanza kampeni kwa kugawa fulana jambo ambalo alisema ni kwenda kinyume cha taratibu.

"Kwa sasa watu wanaruhusiwa kutangaza nia za kuwania nafasi za uongozi na siyo kufanya kampeni."

"Wapo baadhi ya wanaotangaza nia za kugombea na kuanza kampeni kwa kugawa 'T-shirt' (fulana) jambo hili wakati wake bado," alisema Pinda. Kuhusu kilimo, Pinda alihimiza kilimo cha mtama akisema kuanzia mwaka ujao kilimo cha zao hilo kiwe ni lazima na siyo hiyari.

Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi ya umwagiliaji ili kuwezesha kilimo na kupatikana kwa mazao ya kutosha ya chakula na biashara.

Pinda ambaye awali, alipokea kilio cha wananchi kuhusu kukosekana kwa magunia na kamba kwa ajili ya zao la tumbaku aliahidi kuwa serikali itafanya kila iwezalo kuwaondolea kero hiyo na kuahidi kwamba bei ya tumbaku itakuwa nzuri muda si mrefu.

Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini walisema maswali ya waziri mkuu yalionyesha wazi kuwa anawapigia kampeni wakati yeye mwenyewe alikwishaonya kuwa mtu yeyote asifanye hivyo kwa vile wakati wake haujafika.
Walisema Pinda yuko kwenye ziara ya kiserikali lakini anafanya kazi za chama kwa kutumia gharama za serikali jambo ambalo walisema si sahihi.

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Postagem Anterior Próxima Postagem