

Ninachojiuliza hapa ni kwamba ni kwa nini wasitujengee misingi ya kuweza kujitegemea kuliko kutupa fedha na kisha kutupumbaza kuwa sisi ni masikini tunaohitaji kusaidiwa kila saa na dakika?
Kwa nini wasitujengee viwanda vya kusafisha na hatua nyingine sipasayo madini kabla ya kuingia sokoni?
Kwa nini wasituboreshee viwanda vyetu ili tutumie malighafi lukuki tulizo nazo hapa nchini?
Kwa nini wasiboreshe njia za mawasiliano kama mabarabara ili maeneo mbalimbali yafikike kwa urahisi na kuwezesha urahisi wa biashara?
Hapa kuna mengi ya kujiuliza, yapo mengi.
Binafsi nina mashaka sana na misaada hii. Si ya kutusaidia bali yazidi kutukandamiza na kuzidi kuitwa masikini. Najiuliza serikali yetu itaishi kwa kusaidiwa tu hadi lini?
Badala ya kutuwezesha kupata fedha kwa kutumia rasilimali tulizo nazo, wao wanatupa hela kiasi, kisha wao wanazitumia rasilimali zetu, wanarudisha maradufu ya walichotoa kama msaada.
Tanzania ni kama kampuni ambayo nchi za Magharibi zina vipande vyao vya hisa, ambapo kila mmoja anachukua mafao yake kwa kadiri ya hisa zake.
Jamani, tuwezeshwe kupata fedha kwa kutumia rasilimali tulizo nazo na si kwa kudanganywa kuwa tunapewa misaada kumbe ni shukrani kwa kuwaruhusu kutumia rasilimali zetu kwa manufaa yao zaidi.