UCHAGUZI KENYA SASA NI VITA

JOTO la kisiasa nchini Kenya linazidi kupanda. Ikiwa ni chini ya miezi minne sasa kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa rais na wabunge nchini Kenya, tayari wananchi wa Kenya sasa wanashuhudia kwa mara nyingine wanasiasa wa vyama vya upinzani wakirudia makosa ambayo yamekuwa yakitumiwa na chama kilichoko madarakani kupata ushindi kirahisi. Uchaguzi huo, kwa mujibu wa ratiba ya awali, unatarajiwa kufanyika Desemba, mwaka huu. Lakini dhambi ya siasa za kikabila imekwishaanza kuwatafuna Wakenya, ingawa ukabila ni mtaji mkubwa kwa wanasiasa wa Kenya kufikia malengo yao, lakini safari hii, Rais aliyeko madarakani, Mwai Emilio Kibaki, anaonekana kutumia kila nafasi ya udhaifu wa wapinzani wake kuhakikisha anapata ushindi utakaomhahakishia kuendelea kuliongoza taifa hilo katika kipindi kingine cha miaka mitano. Ni jambo lililo dhahiri kwamba, uvumi uliopo sasa wa Rais Kibaki kuingia katika ushirikiano wa kisiasa na Rais wa zamani wa taifa hilo, Daniel arap Moi, ni kete nyingine muhimu inayomhahakishia kuibuka mshindi katika uchaguzi huo, ingawa wanasiasa hawa hawatoki kabila moja. Jambo jingine ambalo linaonekana kumpa ahueni kubwa Rais Kibaki dhidi ya wapinzani wake, ni msuguano unaoendelea ndani ya kundi la upinzani lilikokuwa na nguvu, la Orange Democratic Movement of Kenya (ODM). ODM imeingia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa baada ya wanasiasa vigogo wa chama hicho kushindwa kuafikiana ni nani kati yao asimame kugombea urais akipambana na Rais Kibaki, hata hivyo, Kalonzo Musyoka aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, juzi alipitishwa rasmi kuwania urais kwa tiketi ya ODM-Kenya. Alimshinda Julia Odhiambo. Udhaifu huu wa kambi ya upinzani unaonyesha kuwa Rais Kibaki atakuwa na nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo ingawa ushindi wowote katika chaguzi nyingi za Kenya unategemea zaidi uungwaji mkono wa kikabila. Wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa, wamekuwa wakieleza kuwa mara kadhaa, matokeo ya chaguzi za viongozi wa ngazi mbalimbali nchini Kenya zimekuwa zikitegemea zaidi uwezo wa mgombea kushawishi uungwaji mkono wa kikabila na si vinginevyo.

Na hilo linashuhudiwa pia katika upatikanaji wa maendeleo ya sehemu mbalimbali za nchi hii kwa vile wanasiasa hulipa fadhila kwa kabila lililowaunga mkono na kuwaweka madarakani. Wakenya wenyewe wamekuwa wakiamini kuwa kama ingekuwa ni kuandaa mabilamu ya vipaumbele, ukabila ungekuwa bilamu lenye umuhimu mkubwa katika siasa za nchini mwao. Mawazo, sera na itikadi, vingekuwa katika mabilamu ya nyuma. Hata hivyo, Rais Kibaki anaweza kujikuta katika wakati mgumu iwapo wapinzani wake wataamua kutumia kushindwa kwa serikali yake kutekeleza ahadi zake wakati akiomba kuchaguliwa Rais wa nchi hiyo na hata baada ya kuingia madarakani akiwa ndani ya muungano wa National Rainbow Coalition (NARC).
Wapinzani wa Kibaki wanaelezwa kufahamu fika kuwa yuko katika nafasi ya juu kuliko mtangulizi wake, Moi. Amefanikiwa kukuza uchumi, ameongeza wigo wa kidemokrasia, na amefanikiwa kutekeleza mpango wa elimu ya msingi bure. Na kutokana na hili, Moi ametangaza kumuunga mkono Kibaki, badala ya mgombea wa chama alichokiongoza kwa miaka yote, KANU.
Lakini pia, wapinzani wa Kibaki wanatambua kuwa amefanikiwa katika kuanzisha mfuko wa maendeleo ya jimbo, ingawa baadhi wamekuwa wakidai kuwa hilo amelipa kipaumbele zaidi kwa vile hata yeye ni mbunge. Jambo ambalo hata hivyo haliwezi kuharibu kwa kiwango kikubwa sifa yake hiyo.

Jambo jingine ambalo linaonekana kutafutiwa namna ya kulieleza kinyume kwa wapiga kura ili kupunguza umaarufu wa Kibaki ni mafanikio yake katika ukusanyaji wa kodi. Kibaki anafahamika kwa kufanikiwa kwake kuziba baadhi ya mianya iliyokuwa ikiwawezesha baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kodi. Kwa upande mwingine, wapinzani wa Kibaki huenda wakajenga hoja za kumshambulia kama kiongozi aliyeshindwa kudhibiti usalama wa raia na mali zao. Jambo kubwa linalotarajiwa kutumiwa na wapinzania katika kujenga hoja hii kwa wapiga kura, ni kushindwa kwake kudhibiti makundi ya kihalifu ambayo yamesababisha maafa makubwa kwa wananchi wa Kenya pamoja na mali zao. Iwapo wapinzani watatumia hoja hii, Kibaki anaweza kuwa na wakati mgumu kuipangua kwa kuzingatia kuwa mpaka sasa kundi la Mungiki limekwisha kuua Wakenya wengi huku serikali ya Kibaki ikionekana ikionyesha kila dalili za kushindwa kulidhibiti kundi hilo. Wananchi wa Kenya wanaweza kumsuta Kibaki kwa kile kilichofanywa na vyombo vya usalama vya serikali yake baada kuzinduka kutoka usingizini na kuanza kupambana na kundi hilo ambapo wana usalama wao walijiingiza katika hatua za kuua hata raia wanaoelezwa kutohusika na genge hilo. Kundi la Mungiki ambalo lilianzishwa mwaka 1988, lilipigwa marufuku mwaka 2002, lengo la kuanzishwa kwa kundi hilo lilikuwa kumuondoa madarakani rais wa zamani wa Kenya, Daniel Arap Moi. Kuanzia wakati huo limekuwa likitumia itikadi zilizotumiwa wakati wa uasi wa Mau Mau dhidi ya utawala wa Uingereza katika miaka 1950. Kwa namna uhalifu wa kundi hilo ulivyoripotiwa nchini Kenya mauaji mengi yalifanyika katika kabila linaloongoza kwa ukubwa nchini humo la Wakikuyu. Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa siasa nchini Kenya, hawaoni kama hilo ni suala linaloweza kumuangusha Kibaki kisiasa. Hii ni kutokana na imani waliyonayo Wakenya wengi kuwa ingawa mauaji mengi yaliyofanywa na kundi hili yalikuwa katika jamii ya Wakikuyu, lakini haitarajiwi kama walioathirika kwa kiasi kikubwa wataamua kumuadhibu Kibaki kwa hilo. Suala la kuundwa kwa katiba mpya, nalo linaweza kuwa msumari wa moto utakaotumiwa na wapinzani katika jitihada zao za kumng’oa Kibaki madarakani. Madai ya kuundwa kwa katiba mpya ni kilio cha Wakenya cha muda mrefu sasa, na kwa hakika kushindwa kuundwa kwa katiba mpya kumesababisha hasira kwa Wakenya wengi. Ingawa kuna ukuaji wa uchumi, tatizo la kutokuwepo kwa usawa katika kugawana keki ya taifa nalo linawatafuna Wakenya wengi. Kama ilivyokuwa katika serikali zilizopita pengo kati ya maskini na matajiri limeendelea kuongezeka kwa kiasi kikubwa katika nchi hii inayofuata mfumo wa kibepari tangu ilipopata uhuru wake. Dhambi kubwa ambayo Kibaki anadaiwa kuirithi kutoka kwa rais aliyemtangulia ni kuthubutu kuua demokrasia ya vyama vingi. Kibaki, licha ya kuingia madarakani akitokea katika muungano wa vyama vya upinzani, baada ya kuingia madarakani, kama walivyo watawala wengi wa Afrika, pia anahusishwa na dhambi hii ya kuwakandamiza wanasiasa na wafuasi wa vyama vya upinzani. Kumekuwa na vilio vya kila aina kutoka kwa Wakenya wenyewe kuwa, kambi ya upinzani nchini humo imekuwa ukitazamwa kwa jicho la husuda na kumekuwa na juhudi za makusudi za kuizoretesha. Kinachotajwa zaidi ni tabia ya Kibaki baada ya kuingia madarakani kujaribu kuua vyama vingi kwa kuvipokonya wabunge. Kushindwa kwa kura ya maoni ya kikatiba, pia kunatoa nafasi kubwa kwa wapinzani kumbana Kibaki katika jitihada zake za kuendelea kubakia madarakani. Kwa mtazamo wa haraka haraka ni wazi kuwa wapinzani watatumia suala hili kama moja ya fursa watakazojengea hoja zao za kisiasa, kwamba ‘Kibaki ametunyima katiba mpya kwa sababu anahofia kuwa itamgeuka’. Moja ya mapendekezo katika mabadiliko ya katiba ni kumpunguzia rais madaraka, jambo linaloelezwa kuwa limekuwa likimnyima usingizi Kibaki. Hivyo ni wazi kwamba wapinzani watajaribu kuangalia udhaifu wa Kibaki. Watawaeleza wapiga kura kuwa japo mkongwe huyo wa siasa za Kenya bado angali madarakani na anataka kuendelea kuwa madarakani, ameshindwa kuleta mageuzi ya bunge yaliyokuwa yakitamaniwa na Wakenya wengi. Hata hivyo, ni kazi ngumu kwa wapinzani kufanikiwa hasa kutokana na kusambaratika kwa muungano wao. Ilikuwa rahisi kwa wapinzani kutumia fursa hii kumbana Kibaki, lakini juhudi hizi zingefanikiwa zaidi iwapo wangekuwa kitu kimoja, jambo ambalo sasa ni kama ndoto baada ya Chama cha ODM kilichokuwa kikionyesha kuwa na nguvu, kugawanyika na kuwa makundi mawili. Kundi la ODM ambalo linaongozwa na kambi ya Raila Odinga na lile la ODM –Kenya linalodhibitiwa na kambi ya Kalonzo Musyoka. Haya yote ni dalili za wazi za kushindwa kwa wapinzani katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwaka huu. Hili linatokana na ukweli kwamba siri ya ushindi katika chaguzi nyingi zinazofanyika barani Afrika ni vyama vya upinzani kuungana. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa muungano wa NACK ambao ulikiondoa madarakani Chama cha KANU chini ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Daniel arap Moi. Lakini kwa sababu sasa wamegawanyika, basi kuna shaka kubwa kuwa hawatafua dafu kwa Kibaki hata kama watabeba hoja nzito kwenda nazo kwa wapiga kura kwa vile mgawanyiko wao unatabiri kushindwa hata kabla ya uchaguzi kwa sababu yatari wamekwishampa nguvu Kibaki. Kuna dhana miongoni mwa viongozi wa Afrika kuwa rais aliye madarakani siku zote ni mshindi. Sababu za kusema hivyo ni kwamba; ana vyombo vya habari vya umma ambavyo viko upande wake, wapo watu wengi wenye ushawishi ambao siku zote hutaka kujitengenezea mazingira ya ulaji katika serikali ijayo iwapo watashinda kwa kuvuna tenda na kandarasi mbalimbali za serikali.

Hii inafanya iwe ngumu kumshinda rais aliyepo madarakani. Iwapo ODM ingekuwa hakijagawanyika, swali la msingi kwa chama hicho lingekuwa ni nani atasimama kwa tiketi yake kuombea urais? Lakini kwa sababu mgawanyiko umeishatokea na kuibuka vyama viwili cha ODM-Kenya chini ya Kalonzo Musyoka na ODM chini ya Raila, ni wazi kuwa wote hao watakuwa wagombea wa kiti cha urais na hii ndiyo ishara ya wazi kabisa ya Kibaki kuendelea kubaki madarakani. Bila shaka hivyo ndivyo kwani, mgawanyiko ulitokea kwa njia ya uhasama uliosababisha viongozi hao wawili kutoleana maneno makali, jambo ambalo linaashiria kuwa sasa upinzani ni baina yao kwanza kabla ya kumkabili Kibaki. “Hatua aliyochukua Odinga ni usaliti na ni afadhali ameondoka,” alisema Musyoka mara baada ya Odinga na kambi yake kutangaza kujiondoa ndani ya chama. Hata hivyo kuna wanaosema kwamba bado kunaweza kuwa na mgawanyiko zaidi iwapo Kalonzo Musyoka na Uhuru Kenyatta watakuwa pamoja na kila mmoja akataka kuteuliwa ili kukiwakilisha chama katika kugombea urais. Mgawanyiko wa ODM-K ni taswira ya mgawanyiko uliolikumba vuguvugu la Ford (Ford Movement) mwaka 1992 wakati Keneth Matiba aliposhindwa kuelewana na mzee Jaramog Oginga Odinga na chama hicho kugawanyika katika makundi ya Ford Asili na Ford Kenya, mgawanyiko ambao ulisababisha upinzani kushindwa katika uchaguzi wa rais na wabunge. Pamoja na yote hayo, Kibaki anayo turufu nyingine ambayo ni Rais Mstaafu Moi, mkongwe mwingine wa siasa za Kenya.

Inafahamika wazi kuwa kama ingekuwa utashi wake Moi, angependa kuona Uhuru Kenyatta akiwa rais wa Kenya. Lakini kwa sababu Uhuru alishindwa kufanya hivyo katika uchaguzi uliopita, Moi sasa anaona mchuano utakuwa baina ya Kibaki, Musyoka na Odinga, na hakuna utata kuwa anapendelea kumuona Kibaki akibaki madarakani kuliko Raila Odinga au Musyoka kuwa viongozi wa Kenya.

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Postagem Anterior Próxima Postagem