UTAMADUNI WA KISWAHILI: WILAYA YA KUSINI-UNGUJA

Utamaduni wa Kiswahili
Wilaya ya Kusini-Unguja

Hadi hivi sasa, kitabu pekee ambacho kimeandikwa kuhusu UTAMADUNI WA WASWAHILI ni kitabu cha Ireri Mbaabu wa Chuo Kikuu cha Kenyatta. Juu ya gamba la kitabu hicho, Mbaabu anaueleza upeo wa jitihada zake kuwa kazi yake imekusudiwa wanafunzi wanaosomea shule za upili nchini Kenya. Ama, Utamaduni unahusu mila, asili, jadi, na desturi za mavazi, vyakula, imani, tabia, na maisha ya jamii kwa jumla. Mwalimu Mbaabu anasisitiza katika kuwaaidhi wanafunzi wake kwamba utamaduni ndio msingi wa fasihi. Sura nane za kitabu hicho zimeeleza mengi juu ya Waswahili wa mwambao wa Kenya, Uislamu ukipewa nafasi ya kipekee katika maana ya Mswahili. Malezi ya Kiswahili yameelezwa kutilia sana mkazo dhana ya heshima katika mapana yake.

Vyuo vya Kurani na Maulidi na Kumbini ni taasisi mbili zilizoelezea makuzi na malezi ya Kiswahili. Kazi ya Waswahili ni pamoja na uvuvi, ukwezi, ukulima, usafiri wa baharini, biashara, ufundi mbalimbali pamoja na uundaji wa vyombo vya bahari n.k. Kazi ya uvuvi imepewa maelezo mengi kwa kuwa ina uzito wa kipekee katika maisha ya Waswahili. Kwa mfano, mitego ya samaki aliyoipata mtafiti ni pamoja na thasi, sonyi, lasha, - mitego hii yote ya majarifa hutumika sana usiku. Uzio ni aina ya pili. Aina ya tatu ni nyavu za mikono. Shipi ni aina ya nne. Bunduki-mshale maalumu wa kupigia samaki baada ya kupiga mbizi majini. Kimia ni aina ya sita. Kuvua kuna vyombo na nyakati zake pamoja na itikadi na mbinu mbalimbali.

Ndoa na Harusi: Uswahilini ni taasisi ya kwanza kwa uzito wa maisha ya kila siku ya mtu. Ubikira ni ada kubwa sana kwa wasichana wa Kiswahili kabla ya kuolewa kwani ndoa ndicho kitovu cha maisha ya Waswahili. Ni desturi iliyoenea mwote Uswahilini, kwa wazazi kuwa washauri wakuu wa ndoa za watoto wao. Kuna hatua kadha wa kadha tangu mtu aposapo hadi kutoa mahari na kufunga harusi. Chuo hicho huwashirikisha makungwi na masomo katika kuwaelekeza na kuwafundisha wari harusi kabla na baada ya harusi. Kwa waumini wa kweli wa Uislamu sharia za Kiislamu huwa ndicho kigezo pekee cha kuendeshea maisha ya ndoa.

Nordic Journal of African Studies Mazishi: ni taasisi ya kuwarejesha waja walikotoka, ama na kuwakumbusha walio hai juu ya marejeo hayo kwa Mola wao. Msiba wa Kufiliwa huwa ni faradhi-kifaya kwa Waislamu wote wa ujiranini. Huzuni za kufiliwa huwa ni za wote na kazi kubwa ya majirani na marafiki ni kuwafariji wanandugu waliofiwa. Kazi zote, tangu utoaji wa habari za kifo, uchimbaji ufuo, uoshaji, uchimbaji kaburi, kupatikana kwa tusi, uchukuaji wa jeneza, uzikaji na salla zote za kumsalia maiti ni za jumuiya. Watu wote jumuiani lazima wahusike kwa namna moja au nyingine. Huzuni ya kifo, kwa msingi huchukua siku arubaini. Baada ya hapo hufuata ada ndogo ndogo za duaa na kufyagilia mavani kila mara na kila mwaka, daima.

Ushirikina: ni sura ya mwisho katika kitabu cha Mbaabu. Waandishi wengine wangeweza kuiita sura hii Itikadi. Yeye ameanza sura yake na taarifa ya jumla juu ya Ushirikina. Ameonesha kuwa jambo hili si la Waswahili tu bali ni la watu wote hata Wazungu na si la Waislamu tu bali ni la Wakristo pia. Itikadi ni taasisi iliyo hai katika tamaduni za jamii zote za wanadamu. Ushirikina ni sehemu ndogo katika itikadi za watu. Uislamu na Ukristo hazifunzi wala kuhimiza itikadi hii. Lakini baadhi ya waumini hujikuta wamejaa tele ndani ya uwanja huu wa maisha. Itikadi za Waswahili wa mwambao wa Kenya ni pamoja na imani ya kuwepo pepo - majini, mashetani n.k; nguvu na uwezo wa pepo hao katika kulinda mashamba, mali, miji, kusaidia kutibu maradhi, na mashetani kuroga n.k. Itikadi hizi zina nafasi katika upwa wote wa Waswahili. Pamoja nazo, Waswahili wana mila kama vile ya miiko mbalimbali. Mifano: kula gizani ni kula na shetani. Kunywa maji msalani mtu huwa mwongo. Bundi akilia juu ya nyumba anatangaza kifo n.k. Mbaabu anamalizia sura hii ya mwisho wa kitabu chake na maneno haya: `Itikadi ... zina mafunzo mengi yanayostahili kuhifadhiwa na kuzingatiwa ' (uk.49). Kazi kubwa ya kitaalamu juu ya utamaduni wa Kiswahili, ambayo tunaijua hadi sasa ni tasnifu ya udaktari wa falsafa iliyoandikwa na mwalimu Sengo kuhusu Sanaajadiiya ya Visiwani. Mwandishi wake alivitalii visiwa vya Pemba na Zanzibar kwa utafiti wa kina na kuibuka na hoja za kuueleza utamaduni wa Waswahili wa Visiwani kwa kuheshimu utata uliosababishwa na Bahari ya Hindi. Waswahili wenyewe wana michanganyiko, tangu ya maumbile, damu, historia, asili, sababu, matukio, itikadi, imani n.k. Bahari ya Hindi, historia ndefu ya Uislamu na lugha ya Kiswahili, ni baadhi ya sababu kuu za kuwafanya Waswahili kujihisi wamoja kilugha, kiutamaduni na kihisia. Uafrika asilia umepewa nafasi ya mwanzo katika haki na hadhi ya Waswahili. Suala la ugozi lisitazamwe kisiasa tu kwani kimaumbile watu tumepakwa rangi mbalimbali ili tutambuane na tuelewane kirahisi katika kuendesha mambo yetu ya kila siku maishani. Ama mtafiti wetu huyu wa sanaajadiiya ya Visiwani amekiri katika aya yake ya mwisho tasnifuni kuwa kazi yake kubwa haikuwa kujaribu au kugeza kutoa jawabu za mwisho na za pekee kuhusu masuala ya utatanishi wa Bahari ya Hindi na Sanaajadiiya ya Kiswahili. Juhudi zake ziliishia katika kupendekeza hoja za kurahisisha tafiti za baada yake zitakazolihusu eneo hili zito na tata la mwambao na ulimwengu wa hadithi-jadiiya za Pemba na Unguja. Kazi nyingine ambazo zimefanywa kuhusu vipengele vya utamaduni wa Kiswahili ni pamoja na Tungo Zetu , kitabu pekee hadi sasa hivi ambacho kimezama kitaaluma na kitaalamu kuhusu Msingi wa Mashairi na Tungo nyinginezo. Mbali na mihemko binafsi ya uandishi kuhusu ugozi, Uswahili wa Waswahili na baadhi ya matukio ya Zanzibar ya 1964, Bwana Ibrahim Noor Shariff kajitahidi sana kueleza mapisi ya Waswahili na mambo yao. Kaweza kutufunza wengi juu ya urudhi yaani mipango ya tungo na kumkosoa Sheikh Kaluta Amri Abeid katika kitabu chake cha Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri . Kuna mawimbi ya mihemuko dhidi ya juhudi za mwandishi K.A. Abeid lakini inarekebika bahari ya fikira za mhakiki inapotulizana katika kurasa za mbele. Ama sasa wasomaji wengi tunajua tarehe ya urudhi, utendakazi wa tungo, upungufu katika maelezo ya tungo na mijadala mbalimbali kuhusu kipengele cha ushairi, fani ambayo ina mapisi marefu sana katika Utamaduni wa Kiswahili. Kwa maneno yake mwenyewe, Bwana Shariff anakiri kuwa, "Iwapo ni kweli kwamba bahari ya tungo za Kiswahili ni ya maji makuu, basi ni wazi kabisa kuwa yaliyozungumzwa humu ni maelezo ya kimuhtasari tu kuhusu fasihi hiyo." (uk. 213). Marehemu Shihabuddin Chiraghdin hapaswi kusahaulika katika watenzi wa kazi bora za lugha ya Kiswahili na Utamaduni wake. Ama makala yake "Kiswahili na Wenyewe" yangelingana naye kwa hija, haja na jiha, uzito wake ungekuwa mkubwa zaidi. Hata hivyo, yeye aliweza kujenga msingi madhubuti uliothibitisha kweli yakinifu kwamba Waswahili ni watu hai na hao ndio wenye lugha ya Kiswahili. Sisi wengine sote ni watumiaji na hatuna budi kurejea kwao - wawe na "vibandiko" vyao ama wasiwe navyo - kujifunza kutoka kwao na kujiimarisha katika utajiri wa Kiswahili asilia. Uswahili hivi leo si kinyang'anyiro tena. Katika mlolongo mrefu wa waandishi wa kazi zetu, Maalim Haji Chum amepewa fursa ya kutufungia dimba. Ama yeye kashughulika sana na tafiti za lugha ya Kikae au Kimakunduchi na Utamaduni wake. Kwa watafiti wa Taasisi ya Kiswahili na lugha za Kigeni, Zanzibar, hayuko anayemkaribia kwa kuwa na data zake mwenyewe ambazo kajituma azipate ili aziandikie mabuku. Katika shairi lake la "UTAMADUNI UDUMU," Maalim Haji Chum anatuwaidhi: Kuna nyingi simulizi, ambazo zatia hamu Za kale na siku hizi, kuzitunza ni muhimu Tusiige upuuzi, ja kuabudu mizimu Utamaduni udumu, vizazi hadi vizazi. Mtafiti ameziendea mbio simulizi hizi na anazo za kutosha. Maandishi yake mengi yangeshakuwa vitabu hivi leo kama si wimbi la utatanishi katika mashirika ya uchapishaji. Ama katika mswada huu tunaoufanyia kazi hivi sasa, Maalim Haji Chum anaeleza mapisi ya Wilaya ya kusini, asili za majina ya miji na mitaa, uchumi na mila, lugha ya Kikae, fani mbalimbali, ngoma, jando, daku, shomoo, miongo na sherehe za kuoga mwaka. Kazi hii ni ya msingi sana kwa mtafiti yeyote wa Kikae na Utamaduni wa watu wa Wilaya yote ya kusini. Umuhimu wa kazi hizi zilizotajwa na nyingine nyingi ambazo hazikutajwa (k.m. kazi za Mzee Hamisi Akida, Whiteley, Mnyampala na Shihabuddin, Mohamed Bakari, S.A. Muhammad, Mohamed Abdallah na kazi zote za fasihi) ni mkubwa sana. Tunatumai hivi karibuni tutapata kitabu au vitabu vitakavyojadili Historia ya Kiswahili kwa upana na undani wake, Utamaduni wa Kiswahili kwa kina cha haja na hivyo kuweza kukiegemeza Kiswahili Sanifu katika Kiswahili asilia ili kiwe na mashiko ya kudumu. Kadiri ya mapanuzi na maendeleo yake, makuzi na matumizi yake, Kiswahili Sanifu, kama lugha nyingine zote, sharti kiwe na kwao, kiwe na wasemaji hai wa kwenda kuulizwa kweli ya usahihi wa mambo.

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Postagem Anterior Próxima Postagem