Brazil ni nchi kubwa ya Amerika ya Kusini na pia nchi yenye wakazi wengi kushinda nchi zote za bara hili. Eneo lake ni karibu nusu ya bara lote. Imepakana na Uruguay, Argentina, Paraguay, Bolivia, Peru, Kolombia, Venezuela, Guyana, Surinam na eneo la Guyana ya Kifaransa. Brazil ina pwani ndefu kwenye bahari ya Atlantiki.
Wakazi walio wengi hutumia lugha ya Kireno lakini kuna lugha nyingi kwa sababu ya vikundi vya wenyeji asilia (Waindios) na wahamiaji kutoka pande zote za dunia.
Asilia 75 ya wananchi wanafuata imani ya Kanisa Katoliki. Ndiyo nchi yenye Wakatoliki wengi kuliko zote duniani.
Mji mkuu ni Brasilia, uliopangwa na kujengwa kati ya 1957 na 1960. Mji mkubwa ni Sao Paulo.
Jiografia
Misitu mipana ya dunia inapatikana Brazil katika beseni ya mto Amazonas. Misitu hii inafunika takriban 40% ya eneo la nchi.
Idadi kubwa ya wakazi hukalia maeneo karibu na pwani ya Atlantiki.
Kitovu cha kilimo ni nyanda za "cerado" au savana katika magharibi ya kati ya Brazil.
Miji muhimu
Jiji kubwa ni São Paulo linalofikia (pamoja na mitaa ya jirani) kwenye idadi ya wakazi milioni 20.5.
Majiji ya kufuata ni Rio de Janeiro (wakazi milioni 11.4), Belo Horizonte (wakazi milioni 4.3), Curitiba (wakazi milioni 4), Recife (wakazi milioni 3.6), Fortaleza na Salvador da Bahia (wakazi milioni 11.4 kila jiji) na Brasilia (wakazi milioni 2.2).
São Paulo ni jiji kubwa kabisa linalokua haraka sana. Ni moyo wa kiuchumi wa Brazil wenye viwanda vingi.
Rio de Janeiro ilikuwa mji mkuu wa nchi hadi kuanzishwa kwa Brasilia. Imejulikana kote duniani kutokana na uzuri wa mazingira yake na sherehe ya Kanivali. Ina pia viwanda muhimu na ni kitovu cha utamaduni wa nchi.
Mji mkuu wa Brasilia ulijengwa kama ishara ya umoja wa nchi katika miaka mitatu tu.
Jumla ya asilimia 70 za wakazi hukalia miji mikubwa.
Milima
Mlima mkubwa ni Pico da Neblina (3,014 m juu ya UB) pamoja na Pico 31 de Março (2,992 m) ulio karibu nao kwenye mipaka ya Brazil, Venezuela na Guyana.
Mlima mkubwa wa kusini ni Pico da Bandeira (2.891 m).
Mlima unaojulikana zaidi si mkubwa lakini uko ndani ya mji wa Rio de Janeiro ni Corcovado wenye 710 m. Juu yake kuna sanamu ya Yesu Kristo ambayo ni ishara ya mji.
Mito muhimu
Brazil ina mto mkubwa na mrefu wa dunia ambayo ni Amazonas wenye urefu wa takriban 7000 km. Tawimito yake muhimu ni Río Purús, Rio Negro na Rio Tapajós. Katika mashariki kuna mto Iguaçu wenye maporomoko ya Iguaçu ambayo ndiyo makubwa duniani.
Parana (3.998 km) ni mto mrefu duniani baada ya Amazonas. Unalisha kituo kikubwa cha nishati ya maji duniani cha Itaipú.
Lagoa dos Patos karibu na Porto Alegre ni wangwa kubwa la Brazil lenye 10.000 km².
Ipiranga si mto mkubwa hata kama jina lake linapatikana katika wimbo wa taifa.
Visiwa
Brazil ina visiwa vichache vidogo katika Atlantiki kama vile
Penedos de São Pedro e São Paulo (miamba ya Mt. Petro na Mt. Paulo)
Kisiwa cha matumbawe cha Rocas
Fernando de Noronha
Trindade e Martim Vaz
Visiwa hivi ni sehemu ya mgongo kati wa Atlantiki; hali halisi ni vilele vya milima inayoanza kwenye msingi wa bahari.
Kisiwa kikubwa cha Brazil hakipo baharini bali kati ya mto Amazonas: ni Marajó chenye eneo la 48.000 km² (kubwa kushinda eneo la Uswisi).
Hali ya hewa
Hali ya hewa ni ya kitropiki isipokuwa kusini.
Beseni ya Amazonas ina mvua nyingi. Kwenye milima ya kusini usimbishaji unaweza kutokea kama theluji.
Historia
Brazil imekaliwa na watu tangu miaka 10,000 iliyopita. Waindio waliingia kutoka kaskazini. Hakuna taarifa za kimaandishi lakini akiolojia imeweza kufumbua makazi mbalimbali ya wenyeji asilia.
Ukoloni
Brazil ilikuwa koloni la Ureno kutokana na mkataba wa Tordesillas ambamo Hispania na Ureno zilipatana tarehe 5 Septemba 1494 kuhusu ugawaji wa dunia kati yao baada ya fumbuzi za Kolumbus.
Mreno wa kwanza aliyefika mwambao wa Brazil tarehe 22 Aprili 1500 alikuwa Pedro Alvares Cabral. Makazi ya kwanza ya Wareno ni mji wa São Vicente mwaka 1532. Mji mkuu wa kwanza ulikuwa bandari ya Salvador da Bahia tangu 1549.
Wareno walianzisha kilimo cha miwa wakiwalazimisha Waindio wenyeji kuwafanyia kazi. Walianza kuingia ndani ya bara wakitafuta watumwa kwa ajili ya mashamba na dhahabu.
Hali ya Waindio
Wenyeji walipungua haraka kwa sababu ya kuambukizwa magonjwa ya kigeni wakikosa kinga dhidi yake, halafu kutokana na kutendewa vibaya kama watumwa mashambani.
Wareno walianza kutafuta wafanyakazi penginepo kwa kuchukua watumwa kutoka Afrika.
Mapadri Wajesuiti
Katika hali hii wamisionari Wakristo wa Shirika la Yesu walisimama upande wa Waindio. Walijipatia tamko rasmi la Papa wa Roma la kuwa Waindio ni binadamu kamili, hivyo hawafai kutendewa kinyama. Wakibatizwa na kuwa Wakristo walitakiwa kukubaliwa kama raia yeyote wa Ureno – amri ambayo mara nyingi haikukubaliwa na wavindaji wa watumwa na wenye mashamba.
Mapadri wa Shirika la Yesu walianzisha „reduciones“ yaani vijiji na miji kwa ajili ya Waindio walioishi chini ya ulinzi wao na kutetewa dhidi ya wavindaji wa watumwa. Katika makazi hao Waindio walifundishwa shule kwa lugha za kienyeji na Kireno, na kupata mafunzo wa ufundi mbalimbali. Kwa njia hii mapadre hawa walitawala maeneo makubwa ndani ya bara.
Hali hiyo ilisababisha hasira ya wanasiasa Wareno walioendelea kuwapinga hadi Ureno penyewe. Hatimaye mwaka 1767 hao mapadre Wajesuiti walilazimishwa kuondoka katika Ureno na makoloni yake yote.
Upanuzi wa Brazil
Karne ya 17 na ya 18 iliona kuanzishwa kwa miji mizuri kwa sababu dhahabu na almasi zilivumbuliwa katika misitu ya beseni ya Amazonas. Misafara ya kutafuta hazina hizi zilipanua eneo la Brazil kuelekea magharibi.
Mji Mkuu ulihamishwa kwenda Rio de Janeiro mwaka 1763.
Uhuru 1822
Uhuru wa Brazil ulisababishwa na siasa za Ulaya. Mwaka 1807 Ureno ilivamiwa na Ufaransa ya Napoleon Bonaparte. Mfalme wa Ureno João VI alikimbilia Brazil, Rio de Janeiro ikawa mji mkuu wa dola la Ureno. Mfalme aliporudi Ureno mwaka 1821 alimwachia mtoto wake Pedro utawala wa Brazil. Mwaka 1822 Pedro aliyeona mabadiliko ya kimapinduzi katika makoloni ya Hispana kote Amerika ya Kusini aliamua kutangaza uhuru wa Brazil akiwa mwenyewe mfalme kwa cheo cha Kaisari.