Siri ya Mapinduzi ya 1964
Kama ilivyokaririwa hapo juu njama za serikali ya ZNP ya kuwakamata viongozi waupinzani iliharakisha na kusisimua haja ya kufanya mapinduzi kwa haraka, hata kabla matayarisho ya mapinduzi hayo kuwiva vizuri. Vile vile ile hali ya kwamba ASP ilipata idadi ya voti nyingi zaidi kupita ZNP na ZPPP kwa jumla, iliwafanya ASP kuingiwa na uchungu mkubwa na kwa hivyo wakaamuwa kulipiza kisasi kwa kufanya ghasia kama zile za mwezi wa juni 1961. Lakini mwaka huo, wa 1964, walikusudia kuchoma moto sehemu zote za mjini, yaani stone town, pamoja na vituo vya kuuzia mafuta ya petroli. Wapangaji halisi wa mpango huo hawakuwa Afro-shirazi yenyewe bali ilikuwa Afro Shirazi Youth League, wale waliyokuwa wanachama wa Chama cha Haki za Binaadam na askari polisi wa bara waliyofukuzwa kazi na serkali ya Hizbu pamoja na baadhi ya wafuasi wa Bahai. Mipango yao waliiweka siri sana hata karibu wote viongozi wa juu kabisa wa ASP walifichwa nakutokujulishwa kiini cha mipango yenyewe mpaka dakika za mwisho. Kwani wakati huo uongozi wa ASP ulikuwa umeparaganyika na mchuano mkubwa wa kudai nakupigania uongozi ulifukuta chini kwa chini. Baadhi ya viongozi wa ASP walijihisi wao wakiwa ni Wazanzibari halisi walikuwa na haki zaidi ya uongozi kuliko wale wenye asili ya Kibara ambao vile vile walikuwa hawana elimu. Migongano mikali ilitokana baina ya Wazanzibari kutaka uongozi. Othman Sharif, Hasnu Makame, Saleh Sadalla na Idris Abdul Wakil iliwabidi wajiuzulu tarehe 2 januari, 1964 na kutoka katika ASP. Katika mvutano huo kwenye dakika za mwisho kabla ya Mapinduzi, tarehe 10, 11 januari, Othman Sharif kwa siri kabisa alimuendea Waziri Mkuu Mohammed Shamte na kumpendekezea waunde serikali ya pamoja ya ASP na ZPPP. Wakati huo Othman Sharif alikuwa amekwishapata fununu za Mapinduzi ambayo alikuwa hayataki kwa sababu yalikuwa si ya ASP wala ya Wazanzibari khalisi. Shamte akawakatalia viongozi hao na kuwambia kama walitaka kushiriki serikalini basi iliwabidi watoke katika ASP na waunganishe viti vyao vya Bunge kwenye ZPPP, kina Othman Sharif wakashindwa na masharti hayo. Migogoro hii jinsi ilivyokuwa ya hali ya juu, hata jina la Abdulla Kassim Hanga hatimae lilionekana kukuwemo katika ile listi ya John Okello ya wale Viongozi waliyotakiwa na ASYL kuuwawa mara baada ya Mapinduzi. Kwa hivyo kuuliwa kwa kina Hanga na ASYL baadae sijambo la kustaajabisha. Ushahidi wa kupindukia ulionyesha kwamba Mapinduzi ya 1964 hayakupangwa, kutayarishwa, kuandaliwa au kuongozwa na ASP. Na inaonyesha wazi kwamba viongozi waliyotajwa hapo juu, waliyopendekeza kuu ngana kwa ASP na ZPPP, yaani kina Othman Sharif, walifanya hivyo kutokana na upinzani wao wa kukataa kuendeshwa na Wabara na hiyo ndio sababu wakawa wamekwisha hukumiwa kuuwawa hata kabla ya ghasia hizo kufanyika. Wale waliyoanza suala la kutaka kuleta ghasia, kuchoma moto, kuuwa na kuleta fujo kwa jumla walikuwa ni Afro shirazi Youth league na kiini kilikuwa ni Kamati yawatu 14 yaani: Committee of "14" John Okello* Abdulla Mfarinyaki* Seif Bakari* Abdulla Said Natepe* Yusuf Himid Ramadhan Haji Hafidh Suleiman Khamis Darwesh* Pili Khamis Said Bavuai Said wa Shoto* Mohammed Abdulla* Hamid Ameir Khamis Hemedi
Wageni wengine ambao walishiriki mstari wa mbele wa viongozi katika Mapinduzi walikuwa ni Absolom Amoi Ingen, Matias Simba, Mzee Kenyatta n.k. Nusu ya wanakamati ya "Committee of 14" hao wakiwa wasio na uzalia wa Kizanzibari yaani hao wenye alama ya *. Itaonekana kwamba viongozi wanne wa- juu kabisa hawakuwa ni Wazanzibari na hata Karume alikuwa hayumo katika Kamati hiyo ya watu 14. Karume alitiwa katika kamati hiyo baada ya Mapinduzi na baada ya kuondoshwa kwa Okello na kushika pahala pa Okello. Katika mipango yao ASYL waliandaa Fete usiku wa tarehe 11 kuamkia tarehe 12 januari 1964. Kama ilivyotajwa hapo juu ASYL haikupanga kufanya Mapinduzi bali ilikuwa imepanga kufanya ghasia, fujo na kuchoma moto mjini, Stone Town. Kutokana na hali ya kisiasa ya wakati huo, vyama vyote vya upinzani vilikuwa vimeungana katika United Front. Kutokana na hali hiyo kiongozi mmoja wa Umoja wa Wafanyakazi wa FPTU ambaye vile vile alikuwa ni kiongozi wa Umma Party akadokezewa kwamba kulitaka kufanywa hizo fujo, ghasia na uchomaji moto sehemu za mjini na wale makomred wenye jamaa zao huko sehemu za mjini wawaondoshe. Kiongozi huyo, Ahmed Badawi Qulatein, kutokana na muamko wake wa kinadharia na msimamo wa kimaendeleo akawaonya na kuwashauri viongozi hao wa ASYL kutofanya kitendo hicho, kwani kufanya hivyo kungelikuwa ni sawa na kuwauwa watu wasio na hatia yoyote, ambao karibu wote wakiwa ni wafuasi tu. Kati ya wale ambao wangeliuwawa bure wangelikuwemo watoto, wanawake na wazee, kwa ufupi kungelikuwa kuuwa wananchi ambao hawana hatia yoyote. Zaidi ya hivyo kitendo kama hicho kingeliwafanya wananchi wakauwana ovyo na hatimae wale ambao wangelizianza ghasia hizo wangelikamatwa kufugwa na kuuwawa pamoja na uongozi wote wa upinzani bila ya kuweza kuleta mabadiliko yoyote ya kimaendeelo. Ndipo Qullatein akawaasa kwamba kama wanataka kufanya jambo la maana basi bora wangelifanya "MAPINDUZI" na hatimae wachukuwe serikali na ndipo watapoweza kuleta mabadiliko katika jamii. Kwa njia hiyo kuuwawa kwa watu bure bure kutaepukika na wakati huo huo serikali itapopatikana mfumo wa jamii ulio bora ungeliweza kuzalishwa. Sababu hizo zikawatwanga viongozi hao wa ASYL hasa kwa vile kulikuwa na uwezekano wa wao wenyewe kuuwawa katika ghasia hizo. Ingawaje, wakati huo fununu za ghasia zilikuwa zimeshaifikia idara ya usalama wa serikali ya Hizbu, Karume mwenyewe akiwa mtoaji siri mmoja wapo, kwani alimuendea Ofisa mmoja wa Polisi wa Kiingereza, na kumwambia kwamba amesikia fununu kwamba kulitaka kufanywa ghasia, baina ya tarehe 11 12 Januari, lakini yeye alijikosha kutoka na ghasia hizo kwani alisema kwamba alikuwa hayumo katika mipango hi yo. Kamishna wa polisi akazidharau khabari hizo. Hasa kwa vile serikali ya Hizbu na Polisi wakishughulishwa na kuwaandama Wana Umma, kuwadharau ASYL, na kutoona harakati zozote za Wana Umma, habari hizo wakazidi kuzidharau. Ingawaje mchana kutwa wa tarehe 11 januari 1964, hadi masaa ya usiku kuliwekwa vizinga njia na askari wa PMF kuranda kutwa. Tarehe 11 hiyo magariya PMF (Police Mobile Force) yakiwa yamejaa maaskari yalikuwa yakiranda mchana kutwa sehemu zote za mjini silaha zao walizopewa zikiwa marungu matupu. Usiku ulipoingia askari wa vikosi hivyo vilipoona Umma Party wameingia kulala bila yaishara ya harakati zozote na hao askari wa polisi na wa PMF wakadharau habari hizo na kwenda kulala Mtoni, ambako mara mbili pamema usiku huo kulipigwa matarumbeta ya hadhari. Wale polisi wa Ziwani nao wakajiendea kulala, wakuu wao wa polisi na wa PMF kuchukuwa nyum bani funguo za ghala za silaha. Kosa mojawapo kubwa serikali ya Hizbu ililolifanya ilikuwa kuwafukuza na kuwapa notice ya kuwaachisha kazi polisi waliyokuwa wana asili ya Kibara, baadala yakuwapa watu hao uraiya na kutukuza ujuzi na uwezo wao. Baada ya- kuwawachisha kazi watu hao, serikali hiyo haikuwapa wote wao nauli na kuwa-tayarishiya safariza kurudi makwao, kati yao hatimae, walisaidia katika Mapinduzi kwa ujuzi waliyokuwa nao. Saa sita za usiku wa tarehe 11 Januari, malumpa wa Youth League wakazishambulia kambi ya polisi ya Ziwani na ya Mtoni wakiwa na mapanga, mishare, magongo, mawe, visu na kadhalika. Baada ya kuiteka Mtoni, chini ya uongozi wa Ramadhan Haji, walinyakuwa bunduki za aina ya rifle 200 , sub machineguns 25, Brengun nyepesi 2, bastola nyingi, magrenedi, mabomu ya moshi na risasi. Wakati huo simu baina ya vituo vya polisi zilikatwa, na mfano kituo cha polisi cha Malindi kilipojaribu kuwasiliana na kambi ya Ziwani na Mtoni kilishindwa na hatimae kupeleka gari la polisi la 999 huko Mtoni kwenda kuchunguza. Gari hilo lilipofika huko likakuta Mtoni imekwisha tekwa na askari hao ikabidi wasalimishe roho zao kwa kukimbia na wengine kuogelea baharini kutoka Mtoni hadi mjini. Baada ya ushindi wa ghafla kikosi kutoka Ziwani chini ya Okello, wengi wakiwa na mabunduki bila hata kujuwa namna ya kuyatumia wakaelekea Raha Leo ambako ndiko kulikokuwa Makao Makuu. Baada ya hapo ndipo jina la John Okello likaanz kusikika na vitisho vikaanza kuzagaa visiwani. Kwa kutumia Sauti ya Unguja,Okello aliwatia terra sio wananchi tu kwa jumla, bali hata viongozi wote wa ASP hasa kwa vile walikuwa hawamjui Okello ni nani. Okello alifanikiwa na kuwadanganya walalahoi wenzake kwamba ati alishiriki katika vita vya Mau Mau, na hao kwa upungufu wa maarifa na ujuzi wao kuhusu mapinduzi wakaamini nakumfuata kama vipofu. Sababu ya kutoroka Okello kutoka sehemu mbali mbali za Uganda, Kenya na Pemba na Unguja, inasemekana kwamba alikuwa jambazi, na ndio maana akawa na mwenendo wake wa kikatili. Wana ASYL wakiwa wenyewe wakiongoza na kutekeleza maazimio yao bila ya kushirikisha uongozi wa ASP waliteka Ziwani na Mtoni kwa usiku huo. Baadae huko Makao Makuu Raha Leo ukakuweko uongozi uliyokuwa si wa ASYL. Bahati ni kwamba Aboud Jumbe, Badawi Qullatein, Abdulaziz Twala, na Khamis Abdulla Ameir wakafika hapo na muongozo wa kisiasa ukawa unatolewa, ingawa Jumbe kwa uwoga wake akajiweka chini ya Okello. Ingawaje Jumbe alisaidia katika kupunguza upotovu fulani. Makomred wengine wakashiriki katika ulinzi wa Makao Makuu, Raha Leo, wakiwemo Abdulla Juma, Salim Saleh, Haji Othmani n.k. Hata kabla ya Mapinduzi kuanza Karume alikwisha penya na kukimbilia Dar es salaam, kunusurisha roho yake, katika safari hiyo alimuomba Hanga amshindikize. Babu kwa wakati huo alikuwa akiishi Dar es salaam tokea kukimbia kukamatwa, kama ilivyotajwa huko nyuma. Wakiwa Dar es salaam, Nyerere hatimae akawaita viongozi wote hao watatu, yaani Babu, Hanga na Karume na kuwashauri warudi Zanzibar kwenda kuzuwia watu kuto uwana ovyo . Hapo ndipo Babu, Hanga na Karume wakachukuwa boti la wayahudi Feinsilber na Abramovich tarehe 14 Januari 1964, kuelekea Zanzibar na kushukia Fumba kwa madhumuni ya kuzuiya umwagaji wadamu. Ingawa sehemu mbili muhimu za kiusalama zilikwisha tiwa mikononi, usiku wa baina ya tarehe 11 na 12 ya 1964, bado kulibaki sehemu fulani muhimu za kiusalama ambazo zilishinda kuziteka. Kati ya sehemu hizo ilikuwa ni kituo cha polisi cha Malindi, ambacho Seif Bakari alipewa wadhifa wa kukiteka lakini akashindwa na Gereza la Kiinua Miguu ambalo lilikataa kusalim amri na sehemu hizo kupigana vikali na kusabababisha kuuwawa kwa watu wengi sana waliyoshiriki katika kupindua . Hapo ndipo walipohitajika wenye ujuzi na uwezo wa kupambana katika vita vya kimapinduzi mchana kumekucha kweupe, kwani ASYL walipokwenda Ziwani na Mtoni walikuta askari wamelala na hawana silaha. Lakini baada ya mchana kuingia vituo vyengine havikusalim amri bali vilikamata bunduki na kupigana. Kituo cha polisi cha malindi kilikuwa na askari 70 waliokuwa na silaha kamili na risasi zakutosha, chini ya uongozi wa Inspekta Salim Hakim Khasibi. Askari hawa wakilindwa na makuta ya jumba hilo na kwa kutumilia urefu wa ghorofa, na kituo hicho kuwa njia panda, waliweza kuteketeza watu wengi sana waliyojaribu kukaribia na kutaka kukiteka kituo hicho. Wengi wa wale waliyokwenda kushambulia mwanzoni walikuwa wamakonde ambao walikuwa mara ya kwanza kushika bunduki na walipewa mafunzo ya kutumia silaha na makomred, wengine kati yao walijitwangana risasi wenyewe kwa wenyewe walipo jaribu kumlenga adui. Wengine kama kina Seif Bakari walikamatwa hapo na kuachiliwa na kugeuz wamjumbe wa kupeleka salamu kwa wakubwa zake, kutotambuwa kwamba Seif alikuwa mmoja kati ya viongozi wa juu wa mapinduzi yenyewe. Washambuliaji wengi sana walifariki hapo Malindi na wengine huko gereza la Kiinuwa Miguu. Malumpa- walipoona mambo yanawazidi wakawaomba Makombred wa Umma Party kwenda kuwasaidia kuviteka vituo vilivyobaki. Hapo ndipo kwa mara ya mwanzo kwa Makomred walishiriki katika Mapinduzi kisilaha. Baada ya mashambulizi makali yaliongozwa na komred Amour Doughesh, askari wa kituo cha Malindi wakakimbiana gereza la Kiinuwa Miguu liliposikia makomred, wakiongozwa na Hemed Hilal walikuwa wakijiandaa kuchukuwa dhamana ya utekaji wa ngome hiyo, gereza hilo likasalim amri.
Na baada ya hapo makada wa kikomred wakaendelea kuchukuwana kulinda vituo mbali mbali kama kituo cha simu ya upepo. Kituo hicho kilichukuliwa chini ya uongozi wa Hashil Seif na Kadiria Mnyeji. Aboud Jumbe akiwa ndiye aliyetowa amri ya kukiteka kituo hicho. Ali Muhsin na Mawaziri wake, hatimae, walikwenda kwenye kituo hicho cha simu ya upepo na kusalim amri kwa makomred, Kadiria Mnyeji na Hashil Seif, waliwapatia usafiri na ulinzi wakupelekwa Raha Leo, kwa usalama na amani. Uwanja wa ndege na kituo cha simu vilichukuliwa baaadae na makomred. Hizbu kabla ya mapinduzi, itakumbukwa huko nyuma, kwamba ilikuwa imeshaanza kujitayarisha kutaka kukamata viongozi wa upinzani na kujuwa kwamba vitendo hivyo vingekasirisha wafuasi wa viongozi hao. Kwa hivyo Hizbu inasemekana ilikwisha jitayarisha na mapambano hayo kwa kugawa silaha kwa wafuasi wake.Zaidi ya kugawa silaha waliwatayarisha baadhi ya wafuasi wao washupavu katika mbinu mbali mbali za mapigano. Hizbu ilikuwa na wataalam fulani waliyojifunza mbinu za kijeshi za kigorilla, wakiwa huko Misri na Dhofar. Kati ya askari hao wasiri wa Hizbu walishiriki katika kujaribu kuikowa serikali ya hizbu isiangushwe siku za Mapinduzi na walikuwa wakifanya mazinga ombo yao sehemu za Bubu, Bumbwini na Kianga. Kati ya askari hao kuna waliyowahi kukamatwa mara tatu wakifanya operation hizo siku zile za mapinduzi. Sehemu hizo zilizotajwa hapo juuzi liteketeza washambulizi wengi mno hasa kwa vile Hizbu wa sehemu hizo walikuwa wametayarishwa vizuri na kuwa na silaha madhubuti, kinyume na washambulizi waliokuwa na mapanga, magongo n.k. Ilibidi vikosi kutoka mjini kwenda mashambani huko na kuwateka, baada ya kusalim amri kwao. Serikali ya Hizbu iliwatomeza wafuasi wake waliyokuwa mashamba kutoa roho zao kuhami serikali ya Hizbu, lakini wao viongozi wenyewe walisalim amri na kusalimisha roho zao, kutoroka nchi na kusaliti, wakati wananchi wakiuwana wenyewe kwa wenyewe. Katika mapinduzi watu wengi waliuwawa, na kutoka sehemu zote mbili, wengine wal iuwawa bure na wengine waliuwawa katika mapigano au kwa sababu walishiriki katika mapigano. Kati ya wale waliyouliwa bure ni wa huko Bambi ambako makatili waliyokuwa na msimamo wa kigozi waliwakamata wanawake, watoto kwa wazee, wakawatumbukiza katika visima, kuwatilia makozi, makarare, na madufu, kuwaminia mafuta ya taa na kuwatia moto, watu hao wakiunguwa hali watu wakiwa wazima wazima. Unyamana ukatili huo hauitwi mapinduzi bali ni, ukafiri wa kikatili na wa kinyama kabisa,unaotokana na chuki za kijinga walizotiwa na mwishowe kusahau kama hao waliowauwa ama walikuwa ni ndugu zao, majirani zao au mara nyingine wema waona kuwa waislaam wenzao. Baadala ya kuulani unyama waliyofanyiwa watu wa Bambi, Karume akawatunukia watu hao kwa kuwajengea kati ya nyumba nzuri na bora kabisa baada ya mapinduzi. Mapinduzi yasiyotayarishwa na wanamapinduzi washupavu wenye intidham na muamko wa kisiasa uliyokomaa na wa hali ya juu lazima utakuwa na matokeo ya uovu wa kuvunja sheria, kufanya mambo maovu na machafu. Kwa vile mapinduzi ya 1964 hayakupangwa vilivyo, wahuni wengi na malumpa kadhaa walichukulia nafasi hiyo na kufanya mambo maovu kama vile kuuwa ovyo, kuwaingilia wanawake na wanawari kwa nguvu, kuiba na kuchukuwa ngawira, kuvunja na kupiga watuovyo. Jambo la kusikitisha zaidi ni kuona kwamba katika watu waliyoiba walikuwemo viongozi ambao hatimae wakawa mawaziri na mabalozi, wengine sasa kuwa mawaziri wa serikali ya Muungano na kuna ushahidi kwamba walishiriki kuiba dhahabu na mali nyingi za watu wa Pemba na zaidi ya hayo kushirikiana na Okello kupiga viboko watu wazima wenye heshima zao. Wengi wa hawa watu waliyoonewa walikuwa ni raiya wa kawaida wasiyokuwa na uongozi au uhasama wowote. Bahati nzuri kulikuwa na Makomred ambao vile vile walisaidia kupunguza uuwaji na ukashifishaji wa wanawake, wizi na maovu mengi mengineyo kwa sababu ya elimu bora waliyopewa ya kisiasa. Kushiriki mwishoni katika Mapinduzi kwa makomred kulipunguza balaa jingi kwa sehemu zote mbili za ASP na ZNP.
Haja ya Mfumo halali
Mfumo wa kijamii wa Zanzibar kwa wakati huo ulikuwa unahitaji mabadiliko makubwa, kwani ulikuwa si mfumo wa kihalali wa kuwapa wananchi wote haki sawa. Ulikuwa ni mfumo ambao uliwaweka wengi kwenye unyonge na umasikini wa kusononesha, ilhali wakati huo huo wengine walikuwa wakiogelea katika utajiri. Kutokana na utajiri, ulwa na ubwanyenye, wale watu wa matabaka ya juu walikuwa na kibri kikubwa na kuwadharau wananchi wenzao, kuzidi kuwanyonya na kutumia utawala kulinda maslahi yao dhidi ya haki ya waliyokuwa chini, na wakati huo huo kujidai kuwa ni waislaam wema. Kwa hivyo Zanzibar kwa wakati huo palihitajika mabadiliko ya mfumo wa jamii na mabadiliko yenyewe yaliyohitajika ni kuubadilisha mfumo uliyokuwepo wakati huo, kwa kutumia njia ya kimapinduzi, kwa vile kulikuwa hakuna njia nyengine ya kuleta mabadiliko. Mapinduzi yaliyo hitajika yalikuwa yale yaliyopangwa kwa makini na kuwa na wanamapinduzi wenye siasa ya kimapinduzi makini, waliyopevuka kisiasa, wakiwa na sera za kuleta maendeleo na waliyokuwa wakijuwa nini wakifanya. ASYL walikuwa ni watu wasiosoma na kutowaamini wote waliyokuwa na elimu, kwa hivyo ndio maana hawakutaka kuwashirikisha viongozi wa ASP waliyokuwa na elimu katika mipango ya Mapinduzi yao. Karume mwenyewe alikuwa hakusoma, aliwaamini waliyokuwa hawana asili za Kizanzibari, na kuwaogopa wana ASP waliyosoma, kwa hivyo alielemea zaidi kwa ASYL na ASYL wakamuamini Karume kwa maslahi kwa sababu kama hizo. Youth League katika uongozi wa ASP ikamuarifu Karume pekeyake baadhi ya siri kuhusu mipango yao, ingawa hata naye hawaku mwambia siri zote. Hiyo ndiyo sababu mojawapo, wakati ghasia zilipokuwa zikipangwa wiki mbili kabla ya Mapinduzi, viongozi fulani wa ASP wakajiuzulu kutoka kwenye ASP tarehe 2 Januari, 1964, na hiyo ndio- sababu moja wapo mnamo tarehe 10, 11 Januari1964, viongozi fulani wa ASP, katika dakika za mwisho, wakamuendea Mohammed Shamte kwa madhumuni ya kuunda serikali pamoja ili kuepuka Mapinduzi. Aboud Jumbe alifanya kazi kubwa ya kuwaunganisha viongozi wa ASP na kuwahakikishia kwamba wao ndio watakaondesha hiyo serikali baada ya mapinduzi kwani ASYL walikuwa hawana uwezo huo. Kina Othman Sharif wakakubali hatimae kushiriki katika serikali hiyo, bila ya kujuwa hatari gani iliyowangoja huko mbele. Kuambatana na orodha ya Gazeti Kuu la Serikali la tarehe 24 januari, 1964 orodha ya Baraza la Memba wa Mapinduzi ni kama ifuatavyo: 1. Rais Abeid Karume 2. Makamo wa Rais Abdulla Kasim Hanga ** 3. Mhe. Abdulrahman Mohammed Babu* 4. Mhe. Hasnu Makame* 5. Mhe. Aboud Jumbe 6. Mhe. Saleh Sadalla** 7. Mhe. Idris Abdul Wakil* 8. Mhe. Othman Shariff** 9. Mhe. Abdul Aziz Twala** 10. Mhe. Hassan Nassor Moyo 11. Kamishna wa Polisi - Edington Kisassi 12. Field Marshal John Okello 13. Mhe. Yusuf Himid 14. Mhe. Seif Bakari 15. Mhe. Ramadhan Haji 16. Mhe. A.S. Natepe 17. Mhe. Pili Khamis 18. Mhe. Khamis Hemedi 19. Mhe. Hamid Ameir Ali 20. Mhe. Said Iddi Bavuai 21. Mhe. Siad wa Shoto 22. Mhe. Mohammed Abdulla 23. Mhe. Abdulla Mfarinyaki 24. Mhe. Hafidh Suleiman 25. Mhe. Khamis Darwesh 26. Mhe. Khamis Abdulla Ameir 27. Mhe. Muhammed Mfaume Omar 28. Mhe. Muhsin bin Ali 29. Mhe. Muhammed Juma 30. Mhe. Daud Mahmoud
Viongozi halisi wa ASP wenye alama za ** wameuliwa na wengine wenye alama za * kuhamishwa nchi kama itavyokaririwa wakati suala la Muungano litapojadiliwa katika kurasa za mbele. Kwa siku za mwanzo mara tu baada ya Mapinduzi, Karume pamoja na Viongozi wengi wa ASYL, kutokana na hamasa za Mapinduzi, walionyesha kuwa ni watu wenye fikra za kimaendeleo, baadae kwa sababu za njama za kuunda Muungano viongozi hao wakatiwa fitina na chuki, na kutekwa akili na Nyerere. Katika majadiliano ya siri ya Muungano ilionekana kwamba ikiwa Umma Party pamoja na viongozi waloendelea katika ASP watashiriki katika serikali ya Mapinduzi kikamilifu, basi Muungano wa Nyerere wa aina hii ya leo wa kututawalia usingewezekana. Na kwa kuwaondosha Umma Party na viongozi hao wa juu kabisa wa ASP njiani Muungano ukawezekana kundwa haraka haraka, kama- itakavyakaririwa huko mbele.
Mapinduzi yalitekwa nyara
Madhumuni ya mapinduzi ilikuwa ni kuleta usawa baina ya Wazanzibari, kuondosha dhulma, mapendeleo, ubaguzi, umasini, kuoneyana, kuleta usawa, haki, elimu bora, siha bora, uchumi bora, sheria halali, heshma ya kila Mzanzibari n.k. Mara tu baada ya mapi duzi kulichomoza ishara mbaya dhidi ya matumaini hayo. Kati ya ishara hizo ilikuwa ni uvunjaji sheria kwa baadhi ya viongozi na kuchukuwa sheria mikononi mwao. Sababu moja wapo ya kufanya mapinduzi na kuondosha serikali ya Hizbu ilikuwa, Hizbu ilipitisha sheria zilizo kuwa dhidi ya demokrasia, za kunyima haki huru ya mtu, ya kuunda na kujiunga na chama atakacho mwenyewe, kama vile kufungia chama cha siasa, kama vile kupiga marufuku chama cha Umma Party. Kwa hivyo kunyima haki ya chama cha upinzani, kunyima haki za kuchapisha khabari/fikra huru au mtu kusoma na kuandika fikra huru na azitakazo, kama vile kufungia ZANEWS na Sauti ya Umma, kuzuiliya haki za kusafiri huru kwa watu wenye fikra tafauti na mengineyo, haikuwa mwendo halali na wa kidemokrasia. Hatua hizo za serikali ya Hizbu zilikuwa ni ishara za mwanzo za udikteta, udikteta ambao leo tunaupiga vita. Kwa mshangao mkubwa, mara tu baada ya Mapinduzi, ikaonekana kwamba na ile serikali ya Mapinduzi nayo ilikuwa na njama za kuto heshimu misingi ya demokrasia. Serikali hiyo baada tu ya kushika khatamu, ilianza kwa ishara mbaya, kama vile kuwahukumu vifo viongozi wa serikali iliyopita, adhabu ambayo haifanani na makosa yao na wala wakuwa peleka mahakamani. Kama isingeli kuwa kutetewa kwa vikali sana na A. M. Babu katika Baraza la Mapinduzi basi viongozi hao wa Hizbu leo wangelikuwa marehemu, kwani walikwisha hukumiwa hukumu za vifo. Walipoponea hukumu za kifo ikaamuliwa viongozi hao watiwe vizuizini, na wakawekwa ndani bila ya kupandishwa Mahkamani, hadi miaka 10, baada ya vyama vyao kufungiwa. Ingelikuwa jambo la busara kama serikali ya mapinduzi ingeliwapeleka watu hao Mahkamani, na kupata adhabu kuambatana na makosa yao wakipewa fursa ya utetezi. Kufutwa kwa vile vyama vilivyokuwa vya serikali iliyopita pamoja na kufutwa tena kwa chama cha Umma Party chini ya serikali ya Mapinduzi kilikuwa si kitendo cha kimaendeleo; lingekuwa jambo la maana zaidi pindi serikali ya Mapinduzi ingeliruhusu vyama vya upinzani. Na inakisiwa kwamba kama vyama hivyo vingeliendelea kuweko, kwanza ingelikuwa mfano mwema wakuheshimu haki za kibinaadam na za kidemokrasia na hapana shaka sheria halali zingeheshimiwa, na vifo vya akina Hanga, Othman Sharif, Salum Jinja, Mohammed Humud, Saghir, Ali Othman, Mdungi Ussi, Khamis Masoud, Abdulaziz Twala, Mikidad, Humud, Ahmada, Chwaya, Shindano, Said Nassor na wengi wengineo, vingeepukika pindi watu hao wangelipandishwa Mahkamani na Wazanzibari leo wangeliujuwa ukweli wa dhahiri. Hali hiyo ingeliendeleza uzoefu wa kidemokrasia wa watu kushambuliana majukwaani na katika vikao maaluum na kuwa ndugu wanao sikilizana na kushirikiana kujenga taifa kwa pamoja katika maisha ya desturi, bilaya kujali nani ana fikra gani.
Afro-shirazi
Kama ilivyokaririwa huko nyuma, vyama vyote vya zamani vya Zanzibar vilikuwana migongano ndani ya vyama vyao, Hizbu ilikuwa na kundi la Babu na la Ali Muhsin, ZPPP kuwa na kundi la Mohammed Shamte na Ali Sharif, Umma Party kuwana kundi la Haki na la Wasaliti wakati ASP kulikuwa na kundi la wale waliyoendelea ambalo limeteketezwa, kundi la waliyopigania ukubwa, kundi la waliyokuwa na asiliya Kizanzibari na kundi la waliyokuwa na asili ya Bara. Kundi hili la mwisholilikuwa limetia mizizi katika ASYL chama ambacho ndicho hasa kilichopanga nakuyatekeleza Mapinduzi na ndio maana matokeo ya Mapinduzi yakenda kamayalivyo kwenda. ASP kwa hivyo ikameguka meguka na hatimae kusababisha uuwaji wa kikatili wa viongozi wa ASP uliyopitishwa na ASYL. Kwa vile viongozi wakuu karibu wote wa ASP waliuwawa na wale waliyobakishwa zaidi ya Karume na Thabit Kombo, walikuwa ni viongozi wazee au wa chini kama kina Sh. Daud Mahmoud, Ibrahim Sadalla, Ali Shariff ambao walikuwa ni kama watu waliyotekwa nyara, kwa vile ndugu zao walikuwa wameshauwawa na kwa hivyo wao kuogopea roho zao pindi wangeliteleza. Saa zote walikaa na wasiwasi kama mtu aliyewekewa kisu cha roho. ASP/ASYL iliwadanganya wafuasi wao, kwamba ukabila na utumwa ndizo sababu ya maafa yao yote, lakini viongozi hao hao walivyopata khatamu za utawala baadaya Mapinduzi, walisahau madai hayo na kuwatia wananchi wote kwa jumla, pamoja na wanachama wa ASP, katika maafa makubwa ya kimaisha. Pindi viongozi hao wa ASYL(ASP) wangelichukuwa msimamo wa kijananchi wa kufanya mazungumzo yamasikilizano baina ya wananchi mapema, badala ya kuendeleza siasa ya kikatili, ya chuki na ya kipinga maendeleo, uhasama ugelikuwa ndoto. Kwa njia kama hiyo maovu mengi tungeliyaepuka kutokana na makosa hayo na wapenda maendeleo wasingeliuwawa bure na nchi yetu leo ingelikuwa imeendelea kiwango bora zaidi.
Aboud Jumbe
Ndani ya chama cha ASP na hatimae ASYL, kulitokea maafa mengi, kama vile kuteketeza viongozi wa chama hicho na chama chenyewe tu, bali hata kuwapatisha taabu wafuasi wa kawaida wa chama hicho bila ya kiasi. Wafuasi wa ASP wengi walivunjika moyo sana kuona chama chao wenyewe kikiwatesa. Wafuasi hao vile vile walishangazwa sana kwa kutoshirikishwa katika ujenzi wa nchi yao, katika uongozi wa chama na serikali yao, kutojulishwa au kushauriwa katika jambo lolote lilohusu chama au serikali yao. WanaASP na Wazanzibari wote kwa jumla wana haki yakujuwa nini kilichotendeka katika nchi yao. Wazanzibari wanastahili ukweli kutoka kwa kiongozi mkweli kuhusu mambo mengi ambayo yaliwakuta Wazanzibari. Jumbe kwa vile alikuwa msomi na asiyekuwa kati ya viongozi wa ASYL iliwashangaza wengi kuweza kuepuka haku uwawa kinyume na viongozi wengine wa ASP, kuna fikra tatu kuhusu jambo hilo; moja ni kwamba Jumbe alikuwa myenyekevu sana kwa Karume ambae akitumia manufaa ya kisomo cha Jumbe. Vile vile wakati Hassan Nassor Moyo na Diria walivyowauza kina Hanga kwa Karume walimtaja Jumbe kwamba alihudhiria mikutano hiyo. Karume alipomuuliza Jumbe kwa nini haku ripoti, Jumbe akasema aliliona jambo hilo ni la upuuzi ndio maana haku liripoti kwa Karume. Tafsiri ya tatu inasemekana kwamba Jumbe hakuuwawa kwa sababu yeye kinyume na viongozi wa juu waliyouwawa alikuwa kazaliwa Bara. Pana haja muhimu sana kwa mtu kama Jumbe kujitokeza na kuandika historia ya ukweli ya ASP na serkali ya mapinduzi kama anavyoikumbuka yeye, kabla wauwaji hawajamteketeza. Jumbe alishiriki katika mitihani mbali mbali, kuiona na kuwezakupitia mitihani tofauti, kuishuhudia mi-gogoro ya ndani ya ASP. Jumbe akiwa ni msomi, lakini wakati huo huo aliyezaliwa Bara, kuwa na marafiki na wahisani wasio maafro kama kina marehemu Maalim Zubeir, ni mtu aliyeziona nyuso zote mbili zasarafu. Jumbe anasemekana alipinga msingi wa ghasia za uchaguzi mwaka 1961. Kabla ya uhuru alikuwa na sifa za uongozi wa kitaifa, kushiriki katika mijadala hadhara ya kisiasa na kijamii akichuana na watu waliyokuwa na siasa tofauti na zake. Kama vile majadiliano ya hadhara na A.M.Babu. Jumbe tokea mapema januri 12, 1964 alikuwa pamoja na Umma Party na kuweza kujuwa mchango wao katika mapinduzi. Anajuwa kuhusu vifo vya kina Hanga .Alikuwa kalamu na tupa ya Karume. Baada ya kuuwawa Karume, Jumbe ndiye aliyechukuwa jukumu la kutangaza kifo cha Karume katika radio na kujuwa vilivyo hali ya Viongozi wenzake wakati huo. Baada ya kifo hicho alipambana na kuwa na migogoro mingi na Seif Bakari katika kuwaniya kanda za khatamu za utawala. Jumbe ndiye aliyejaribu kuifufuwa ASP kwa kuitisha Kongres ya mwanzo baada yamapinduzi huko Pemba, lakini jaribio hilo kutofaulu, kwani khatamu za chama zikashikwa na wale wale ASYL. Hatimae Jumbe alifanikiwa kwa kiwango fulani kuwapunguzia Wazanzibari maafa kwa kupunguza nguvu za Baraza la Mapinduzi kwa kuwa sambaza sambaza na kuwaleta vijana wepya serikalini, vijana ambao wengine wao walikuwa wana YASU na wengine kutokuwa wanasiasa hapo kabla, hatimae vijana hao walikuwa ndio shina la utawala wa Jumbe. Jumbe alifanikiwa kwa kiwango fulani kuwarejeshea watu haki zao za kuweza kutoa maoni. Kosa kubwa mojawapo alilolifanya Jumbe lilikuwa ni kufuta Chama cha kisiasa Zanzibar na kuifanya Zanzibar izidi kumezwa, alifanya hivyo kwa kutarajia kupewa Urais wa Tanzania, hatimae. Kutokana na kuzidi kujitambulisha na dini ya kiislaam na kutambuwa mbinu za Nyerere za kutaka kuifanya Zanzibar jimbo, Jumbe, alitanabahi na kuzindukana, na kuchukuwa khatuwa za kuitoa Zanzibar katika Muungano na kwa hivyo akaporopolewa na Nyerere. Haya ni baadhi tu ya mambo ulimwengu unayoyangoja kutoka katika kauli ya kweli ya Jumbe. Historia ya Zanzibar haitokamilika bila ya Jumbe kuichangia kwa ukweli anaoujuwa.
Makosa ya Umma Party
Chama chochote cha kisiasa hakina budi na kufanya makosa ya kisiasa, mara nyengine makosa hayo huwa madogo na mara nyingine huwa makubwa mno. Makosa kama hayo yalifanywa na vyama vyote pamoja na Umma Party na hatimae kusababisha athara kubwa visiwani Unguja na Pemba. Moja katika makosa ya Umma ilikuwa kujiweka nyuma na kuonyesha kwamba wao ni watu wenye roho safi na wasiopapatikia khatamu za utawala, kusahau kwamba wao wakiwa hawatakuwa na uroho wa utawala, kutakuwa na wengine wengi ambao hawatopapatikia utawala tu bali watautumilia dhidi ya maslahi ya umma. Kuogopa kwa Umma Party kushika khatamu za utawala kulitokana na uwoga wa kuhutumiwa kwamba walikuwa na njaa ya utawala, na kwamba badala ya kupigania wanyonge, lile walilolitaka lilikuwa ni ulwa wa kuwatawalia wengine. Mawasiliano mazuri ya Umma Party na baadhi ya viongozi wa ASP pamoja na vyama vilivyoshirikiana na ASP iliwafanya Umma Party kuwa na imani kwamba ASP badaya kupata khatamu za utawala itatawala kihalali na kupitisha haki. Umma Party ilisahau kwamba si viongozi wote wa ASP waliyokuwa na ujuzi au nia safi, na kwamba wengine walishughulishwa zaidi na maslahi yao binafsi. Umma Party haikutarajia kwamba viongozi wa ASP Youth League watawageukia wengi wa viongozi wa ASP, viongozi ambao walikuwa na fikra za maendeleo. Umma Party vile vile, katika jazba na hamasa za kimapinduzi ilisahau kwamba, viongozi wa ASYL ingawa walijitolea kufanya mapinduzi, walikuwa kwanza ni watu wasiyoelewa mambo ya kiserikali na kwa hivyo ilikuwa ni rahisi kubabaika na kulevywa na khatamu za utawala. Umma ilisahau kwamba hawa watu walikuwa wanaupungufu wa ujuzi wa kuendesha serikali. Badala ya kwamba Umma ilikuwa iwahakikishie viongozi hawa wa ASYL kipato na satwa ya kudumu kwa mchango wao katika mapinduzi, waliwawachia kuendesha serikali kama rikwama, wakitarajia kwamba yale mapendekezo ya kimaendeleo waliyoyatowa Umma Party yatatumika katika kuendeleza nchi. Viongozi wa chache wa Umma Party, waliyokuwa na sifa za ubinafsi, walisaliti na kujichukulia jukumu la kuzidi kuwapeleka mbele baadhi ya viongozi wa ASYL, wakijuwa wazi kwamba watu hawa walikuwa hawawezi kuziendesha nyadhifa hizo kama ilivyotakiwa. Badala yake viongozi hao wa ASYL kutokana na upungufu wa ujuzi wao wakawa wana wahka na kuona adui katika kila pembe, na badala ya kuinuwa maslahi ya wanyonge wakazidi kuwakandamiza wanyonge hao hao ambao walidai kuwatetea. Pindi Umma Party ingelihakikisha udhibiti mshupavu wa khatamu za utawala katika mikono halali na madhubuti, basi nchi ingeliendelea kwa haraka na kwa amani. Um- ma wa Kizanzibari usingeliteseka, mauwaji yangeliepukwa, vifungo na kutiwa watu vizuizini kwa miaka hadi kumi kungeliepukika. Utawala wa mashirikiano ya Umma na viongozi wa ASYL na viongozi waliyoendelea wa ASP ungeweza kuondosha uhasama na chuki za kisiasa na hatimae kuleta masikilizano hata na ZNP na ZPPP, pindi ASYL wangeliwahiwa kupewa elimu ya siasa ya mapema na ya kutosha. Wazanzibari wangeliweza kuwa kitu kimoja na pasingekuwa na haja ya Karume kuwa na wasi wasi na kujiingiza katika Muungano bila ya kupenda. Khatuwa za kurekibisha dira ya muelekeo wa nchi zingelifaa kutendeka mapema, yaani muda tu baada ya mapinduzi au hata kabla ya ufanyaji wa mapinduzi yenyewe na hatimae kungeliepusha nchi leo kutawaliwa na kuselelea nyuma. Ingawaje, wakati tu baada ya Mapinduzi palikuwa na migogoro na mifarakano fulani hasa kwa vile baadhi ya watu, kwa jina la Mapinduzi, wal ifanya kila aina ya uovu. Haya mambo hayakuwafurahisha wana Umma, na ikafika hadi baadhi ya wana Umma fulani waka mkabil John Okello na kumwambia awache kuadhibu raiya wasiyokuwana makosa. Wakamueleza Okello kwamba akishindwa na kuzuwiya vitisho nakufanya ukatili huo basi ingelimbidi akabiliane na wana Umma kisilaha ana kwa ana. Okello wakati huo alikuwa akitakabar sana na nchi ilikuwa kama ikiendeshwa na Marais wawili, upande mmoja Karume na wa pili Okello. Wakati huo viongozi wengi, akiwemo na Karume, wakimuogopa sana Okello. Okello inasemekana mara kwa mara akisafiri kwenda Kenya na Uganda kupeleka mali ya ngawira. Safari moja, mwanzoni mwa march 1964, Okello aliporudi kutoka Dar es salaam, akalikuta Baraza la Mapinduzi likimsubiri uwanja wa ndege kwa madhumuni ya kumfukuza nchi. Okello, wakati huo, alikuwa akiogopwa sana kwa hivyo ilibidi waagizwe Makada wa Umma Party wakiwa na silaha kamili. Baada ya Okello kusomewa madhambi yake na Karume, mbele ya memba wa Baraza la Mapinduzi, huko uwanjawa ndege. Makada wa Umma Party waliyokakamaa na silaha mkononi wakamshindikiza Okello hadi ndani ya ndege iliyokuwa ikimsubiri na kumsafirisha kwendea Dar es Salaam na hatimae kurejeshwa kwao Uganda. Absolom Ingen,aliyekuwa makamu wa Field Marshal Okello na kuwa kati ya waliyoogopwa sana na waliyofanya fujo nyingi, utesaji mkubwa na kashfa nyingi baada ya Mapinduzi nae alipotaka kuoondoshwa alitiwa mbaroni na makada wa Umma silaha mkononi na baadae akarejeshwa kwao Kenya. Kama makada wa Umma tokea mwanzoni wangelipewa nyadhifa kama hizo basi wale watesaji na wauwaji wasingelipata nafasi hizo na nchi isingelikwenda mramba. Watu wawili hao, yaani Okello na Ingen, ni kwa wakati huo viongozi wa juu kabisa katika mapinduzi, na ambao wakiogopwa Zanzibar nzima, lakini ilipohitajika makada wa Umma Party waliwatia mbaroni kama mchezo wa mdako. Hayo ni makosa ya Umma Party ambayo yanafaa kujadiliwa ili yaepukwe siku za mbele.